Tag: minimal

  • BM.14.11.\3.6 MLANGO KUHUSU ADHABU YA WIZI

    BM.14.11.\3.6 MLANGO KUHUSU ADHABU YA WIZI

    Hadithi ya Leo, Jumaane, tarehe 29, Mfungo Tano, 1446, H. sawa na tarehe 03, Ogasti, 2024

    SEHEMU YA SITA

    KUHUSU ADHABU YA WIZI

    1236* وَعَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ عَوْفٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ؛ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ  قَالَ: لَا يَغْرَمُ السَّارِقُ إِذَا أُقِيمَ عَلَيْهِ الْحَدُّ. رَوَاهُ النَّسَائِيُّ، وَبَيَّنَ أَنَّهُ مُنْقَطِعٌ. وَقَالَ أَبُو حَاتِمٍ: هُوَ مُنْكَرٌ*.

    1. Imepokewa kutoka kwa Abdulrahman bin Awf **رضي الله عنه akisema: “Amesema Mtume : “Halipishwi mwizi fidia ya kitu alichokiiba, baada ya kupitishiwa hukumu ya kukatwa mkono.” Ameipokea Nasai ila amebainisha kuwa Riwaya yake haikufika kwa Mtume . Abu Hakim anasema: Riwaya hii ni Munkari.

    UFAFANUZI

    Haidithi hii, pamoja na kwamba maana yake ni sahihi kuwa mwizi akithibitika kuwa ameiba na akakatwa mkono wake, haijuzu kumtaka alipe fidia ya kitu alichoiba, ila Isnadi yake ni pungufu, haijakamilika, maana mpokezi mmoja aitwaye Al-Miswar bin Ibrahim bin Abdurrahman bin Awf, hajakutana na Babu yake Abdurrahman bin Awf, lakini katika Hadithi amesema kuwa ameipokea kutoka kwa Abdurrahman bin Awf, ambaye ni babu yake. Hata Abu Hatim ameipokea hivyo hivyo, na kuishia kusema kuwa Hadithi hiyo ni Munkari; yaani haiwezi kukubaliwa kuwa ni maneno yametoka kwa Mtume ﷺ ; maana mtu yeyote akithibitika kutenda hatia na akatiwa adhabu ya Mwenyezi Mungu, hawezi kutakiwa alipe fidia ya kitu alichokiiba, wala kutakiwa arudishe alichokiiba, baada ya kutiwa adabu ya Mwenyezi Mungu. Hivyo, mafunzo yake ni kweli, lakini matamshi yake kunasibishwa kwa Mtume ﷺ siyo kweli.

    YALIYOMO NA YATOKANAYO

    1. Mwizi aliyeiba kitu cha mtu mwengine, ana haki mbili:
      a) Haki mahasusi, nayo ni kitu alichokiiba iwapo kipo; au kutozwa fidia iwapo alichokiiba hakipo, au kutozwa thamani ya alichokiiba, iwapo alichokiiba kimepotea au kimeharibika.
      b) Haki ya Jamii ya Waislamu, juu yake, na hiyo ndiyo Haki ya Mwenyezi Mungu, ya kukatwa mkono baada ya kukamilika masharti na nguzo za kukatwa mkono, au kuaziriwa iwapo hayajakamilika masharti ya kukatwa mkono.
    2. Iwapo kitu alichokiiba kipo salama, kama kilivyokuwa kabla ya kuibiwa, basi wanazuoni wa Kiislamu wameafikiana kuwa ni wajibu kurudishwa kwa mmiliki wa kitu hicho, na hakuna adhabu ya mwizi aliyekiiba kukatwa mkono, bali atatiwa adhabu ya kuaziriwa na kufedheheshwa hadharani.
    3. Haki ya Mwenyezi Mungu, ikithibitika hatia, lazima ipitishwe, ambayo ama ni Adhabu kubwa iliyowekwa juu ya aliyetenda Hatia, au adhabu ndogo, nayo ni kufedheheshwa hadharani, ili ajulikane kuwa ni mtu aliyewahi kuvuka mpaka ya Mwenyezi Mungu, makusudi.
    4. Adhabu za Mwenyezi Mungu kwa Hatia mbali mbali, hazikuwekwa kuwa ni ndiyo lengo lenuyewe, bali ni Onyo na Tahadhari kwa wengine, wasitende hatia husika; hivyo ni wajibu wa kukamilisha lengo hilo la kuzuwia wengine wasitende hatia hiyo.
    5. Haki ya Mwenyezi Mungu haiepukikji baada ya kufikishwa aliyetenda Hatia ya Adhabu, akishafikishwa mbele ya Mwenye mamlaka rasmi ya kupitisha Sharia za Mwenyezi Mungu.
    6. Hakuna junaha kwa aliyetenda hatia ya Adhabu ya Mwenyezi Mungu, kutopitishwa Adhabu ya Mwenuyezi Mungu, KABLA ya kufikishwa mbele ya Mwenye Mamlaka ya kusimamia Sharia, kwa kusamehewa na aliyedhulumiwa au aliye dhuriwa na mtenda hatia.
    7. Inajuzu kwa mtu aliyedhulumiwa au kudhuriwa, kumsamehe aliyemdhulumu au kumdhuru, kama alivyosema Mtume ﷺ : “لا يحل مال امرىء مسلم، إلاَّ بطيبة من نفسه” Haimjuzii mtu kujihalalishia mali ya mtu Mwislamu mwengine, isipokuwa akiridhia kumhalalishia.”

    والله أعلم

    وبالله التوفيق