NINI HUKUMU YA KUVAA HIRIZI AU KINGA

Nimeulizwa, NANUKUU: ‎

‎“Habib Abdulqadir nina suala. Nini Hukumu ya kuvaa hirizi, au Kinga? Na ‎Nini hukumu juu ya mwenye kutengeneza Hirizi hizo? Naomba ufafanuzi wa ‎kina, maana ni tabia iliyozagaa sana katika jamii zetu.”‎

JIBU

BISMILLAH

Neno “Hirizi” lina maana pana, ila maana zote zinalenga katika ‎kumaanisha KINGA, na hivyo hutumiwa kwa kitu chochote kile ‎kinachoaminiwa kuwa ni kinga ya jambo baya, au jambo lisilotakiwa. ‎

Kwa upande wa lugha, hirizi ni hifadhi au kinga ya jambo fulani. ‎Neno jengine linalotumiwa ni ‎حجاب‎ hijab, ‎طلاسم‎ twalsam-twalasim,na ‎عزيمة‎ ‎‎‘aziima-‘aza’im yote yana maana moja ya kukinga, kulinda, kunusuru, ‎kusitiri, kuchunga na kadhalika. ‎

Na ni kutokana na maana hizo ndimo tunapata neno hijabu ‎linalotumiwa kwa upande wa Sharia, kumaanisha vazi la kujisitiri, kwa ‎Kiswahili ni Buibui, au kwa lugha ya siku hizi, ‘abaya. [ingawa hayo ‎yanayoitwa ma’abaya yamegeuzwa, siku hizi, kuwa ni vivutio zaidi kuliko ‎kuwa ni stara au hifadhi ya mwili ‎والله المستعان‎ ] ‎

Kwa upande wa itikadi na imani, hata hivyo, tunapozungumzia Hirizi ‎neno hilo linamaanisha kinga ya zindiko ili usifikwe na jambo fulani. ‎

Iwapo zindiko hilo ni la maandishi maalum, basi maneno mengine ‎yanayotumiwa –hata kwa Kiswahili- ni Talasimu, Azima, Hijabu, Zindiko ‎na Sihiri. ‎

Lakini, iwapo zindiko hilo linahusishwa na kitu maalum, kuwa kina ‎nguvu za kukulinda na jambo fulani lisikufike, basi maneno yanayotumiwa, ‎katika Kiswahili, ni Kago, Ndumba, Tunguri, Ndonga na Kinga. Ni maana ‎hizo mbili: kinga ya maandishi na kinga ya kuamini kuwa kitu fulani ‎chenyewe kina nguvu za kukulinda na jambo fulani au kukulinda na kitu ‎fulani chengine, ndizo nitazozungumzia hapa.‎

A)‎ Hirizi kwa maana ya kinga ya maandishi. ‎
‎ ‎
Kuna maadishi ya aina mbili, yanayo tumiwa katika kuandika hirizi. ‎

a)‎ Kwanza ni maandishi ya majina ya mashetani, majini au michoro ya ‎mazingaombwe ya shaghala-baghala, wakidai kuwa ni kiatu cha ‎Nabii Sulaiman, au Nyota ya kitu fulani, au sura za vitu maalumu, au ‎nambari maalumu, ect., ect. Hizi ndizo zinazoitwa Talasimu, na ‎Hirizi; kwa Kiarabu zinaitwa: ‎تمائم ‏‎ au ‎تولة‎. Hizi ni kufuru. Kiatu cha ‎Nabii Sulaiman si kinga wala si dawa ya kitu chochote; iweje mchoro ‎wake uwe kinga ya jambo lolote lile. Ubahalula. Uzandiki. Ujinga. ‎Ulanguzi wa wadanganyifu wa kuwaibia na kuwala wajinga. ‎Haramu kabisa, bali ni kufuru. Vile vile huitwa ‎رقيا الشيطان‎ au ‎رقي‎ tu.‎

b)‎ Maandishi ya Qur’ani au Majina ya Mwenyezi Mungu na kadhalika. ‎Haya huitwa ‎حجاب الشرعي‎ au ‎الرقيا الشرعيHakuna junaha iwapo ‎maandishi hayo ni Aya za Qur’ani au Majina ya Mwenyezi Mungu, ‎kwa sharti kwamba pasiaminiwe kuwa MAANDISHI HAYO ndiyo ‎yanayo kukinga au kukulinda. Bali mwenye kukukinga na kukulinda ‎ni Mwenyezi Mungu aliyesema maneno hayo. Yaani unatumia Aya ‎za Qur’ani au Majina Matakatifu ya Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya ‎kutabaruku tu, ukiamini kuwa mwenye kukinga na kulinda ni ‎Mwenyezi Mungu, ‎

Mwenyezi Mungu amesema, kuhusu Qur’ani: ‎

‏﴿وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ وَلا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلا خَسَارًا﴾ [الإسراء: 82]‏‎.‎
Na tunateremsha katika Qur’ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa ‎Waumini. Wala hayawazidishii madhalimu ila khasara. (Al-Isra’, 17:82)‎

Na amesema, katika Surat Al-An‘am, Aya ya 155:‎
‏﴿وَهَذَا كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴾ [الأنعام: 155]‏‎.‎

Na hiki ni Kitabu tulicho kiteremsha kilicho barikiwa. Basi kifuateni, na ‎mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemiwe. (Al-An‘am, 6:155)‎

عن محمد بن عبد الرحمن بن أبي ليلى عن عيسى أخيه قال: دخلت على عبد الله بن عكيم أبي معبد ‏الجهني أعوده وبه حمرة فقلنا: ألا تعلق شيئًا؟ قال: الموت أقرب من ذلك، قال النبي صلى الله عليه ‏وآله وسلم: «مَنْ تَعَلَّقَ شَيْئًا وُكِلَ إِلَيْهِ (رواه الترمذي وإبن ماجه )‏

Imepokewa kutoka kwa Abdurrhaman Ibn Abi Layla kutoka kwa Isa ‎kutoka kwa ndugu yake akisema: “Nilimtembelea Abullah bin Ukaym; Abi ‎Ma‘bad al-Juhaniyy, akiwa mgonjwa, akiwa amekaa na Hamza bin Abdil ‎Muttalib (Ami yake Mtume ‎ﷺ‎ ). Tukamwambie kwanini huvai hirizi ‎yoyote ile ya kujikinga? Akajibu kwa kusema: “Mauti yamesha nikaribia ‎zaidi kuliko kufanya hivyo. Na nimemsikia Mtume ‎ﷺ‎ akisema: ‎‎“Atayejifunga kitu (kama hirizi) ataachiwa nacho kimsaidie kama kinaweza ‎kumsaidia.” Ameipokea Tirmidhi na Abu Daud.‎

Wanazuoni wameifasiri kuwa ukivaa kitu chochote kile, basi ‎utaachiwa wewe na kitu chako hicho kikusaidie kama kinaweza ‎kukusaidia; yaani utasokomezwa nacho. Hivyo, ukivaa maandishi ya Aya ‎za Qur’ani basi Mwenyezi Mungu hatokusokomeza kwa asiyekuwa yeye ‎akusaidie, bali atakusaidie yeye Mwenyewe, maana Qur’ani ni maneno ‎Yake, ambayo ameyaelezea kuwa ni dawa na tiba na rehema. ‎

Kwa maana hiyo, atayevaa au kujitundikia Aya za Qur’ani basi ‎hawezi kuachiliwa na Mwenyezi Mungu asaidiwe na asiye kuwa Yeye; ‎lazima atamsaidia Yeye mwenyewe kumtibu, kumlinda na kumhifadhi. ‎Hivyo ndivyo walivyo fasiri wanazuoni wakubwa wakubwa wa Tafsiri za ‎Qur’ani, kama Imam Al-Qurtuby katika Tafsiri yake: ‎الجامع لأحكام الفرآن (10 ‏‏:320 )‏‎ . Wengine ni Twabary, Ibn Kathiir na wengine.‎

عن عمرو بن شعيب عن أبيه عن جده: أن رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم قال: «إِذَا فَزِعَ أَحَدُكُمْ ‏فِي النَّوْمِ فَلْيَقُلْ أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللهِ التَّامَّةِ مِنْ غَضَبِهِ وَعِقَابِهِ وَشَرِّ عِبَادِهِ وَمِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ وَأَنْ ‏يَحْضُرُونِ؛ فَإِنَّهَا لَنْ تَضُرَّهُ». قال: وكان عبد الله بن عمرو رضي الله عنهما يعلمها مَنْ بَلَغَ من ولده، ‏ومَنْ لم يَبْلُغْ منهم كتبها في صك ثم علَّقَهَا في عُنُقِه رواه أبو داؤود والترمذي‎.‎

‎ ‎ Vivyo hivyo, imepokewa kutoka kwa Amr bin Shu‘ayb kutoka kwa ‎Baba yake kutoka kwa Bab u yake akisema: Amesema Mtume ‎ﷺ‎ : ‎Akishtuka mmoja wenu usingizini kutokana na ndoto mbya, basi aseme: ‎أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللهِ التَّامَّةِ مِنْ غَضَبِهِ وَعِقَابِهِ وَشَرِّ عِبَادِهِ وَمِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ وَأَنْ يَحْضُرُونِ؛‎ kwani hatosibiwa na kitu chochote, kile. Na amesema kuwa ‘Abdullah bin ‎Amr ‎رضي الله عنهما‎ alikuwa akiwafundisha dua hiyo watoto wake waisome ‎wanapo shtushwa na ndoto mbaya usingizini, na kwa wale ambao ‎walikuwa bado hawakubalighi, basi alikuwa akiiandika dua hiyo kwenye ‎karatasi na kuikunjakunja na kisha kuitundika shingoni mwa mtoto huyo.” ‎Ameipokea Abu Daud na Tirmidhi.‎

Hivyo, kitendo cha Sayyidina ‘Abdullah bin ‘Amr ‎رضي الله عنهما‎ ‎kunukuu dua aliyofundisha Mtume ‎ﷺ‎ kujikinga na vitisho vya usingizini, ‎na kuiandika kwenye karatasi na kisha kuitundika karatasi hiyo kwenye ‎shingo ya watoto wake wadogo ni dalili kuwa inajuzu kuvaa hirizi ya dua ‎ya kumuomba Mwenyezi Mungu, pekee, na kama dua inajuzu, basi ‎Qur’ani inajuzu zaidi, maana Mwenyezi Mungu amesema kuwa Qur’ani ‎ni dawa, uponesho na rehema kwa Waumini. ‎

Vivyo hivyo, wafuasi wakubwa wakubwa wa Maswahaba wa ‎Mtume ‎ﷺ‎ kama Ataa’, Mujahid na Sa‘id bin al-Musayyib ‎رضي الله عنهم‎ ‎walikuwa wakiwaandikie watu hirizi za Aya za Qur’ani na dua za Mtume ‎ﷺ‎ na kuwapa wazivae kama hirizi. (Muswannaf In Abi shayba, juzuu ya ‎‎3, kurasa 43 hadi 44)‎

Imam Malik ‎رحمه الله‎ amesema: Hakuna junaha kuvaa hirizi za Aya ‎za Qur’ani. Msimamo huo umeelezewa vile vile na wanazuoni wakubwa ‎wakubwa, kama Ibn Hajar katika Fat-h al-Baary Sharh Swahih al-Bukhari, ‎juzuu ya 6, ukurasa 142, alipokuwa akifafanua makatazo ya Hadithi yenye ‎kukemea kuvaa hirizi za talasimu za maandishi yasiyokuwa Qur’ani ,kwa ‎kusema:‎

هذا كله في تعليق التمائم وغيرها مما ليس فيه قرآن ونحوه، فأما ما فيه ذكر الله فلا نـهي فيه؛ فإنه ‏إنـما يجعل للتبرك به والتعوذ بأسـمائه وذكره .‏
Makatazo yote haya ya hirizi za matalasimu ni kuhusu ‎maandishi yasiyokuwa Qur’ani au yasiyokuwa majina ya Mwenyezi ‎Mungu. Ama utajo (Qur’ani) wa Mwenyezi Mungu haukukatazwa; ‎kwani Qur’ani imefafanuliwa na Mwenuezi Mungu kuwa inajuzu ‎kutabaruku nayo na vile vile kujilinda kwa Majina Matakatifu ya ‎Mwenyezi Mungu. ‎

Na kuna Hadithi nyingi sana zinazosema kuwa inajuzu kujizingua ‎kwa Aya za Qur’ani au dua maalumu za kuzingua, ambazo ametufundisha ‎Mtume ‎ﷺ‎ . Na tofauti ya kuzingua na kujilinda, yaani hirizi ya maandishi ‎ya Qur’ani ni kwamba kuzingua ni tiba baada ya kufikwa na tatizo; vile ‎hirizi ni kinga usifikwe na matatizo; ila Aya ni zile zile, na maneno ni yale ‎yale ya Mwenyezi Mungu. Hakuna junaha.‎

Kwa ufupi hakuna junaha kuandika au kuvaa hirizi za maandishi ‎ya Aya za Qur’ani, au dua za Majina Matakatifu ya Mwenyezi Mungu, au ‎hata dua zilizopokewa za kujilinda kutoka kwa Mtume ‎ﷺ‎ . Yaani dua ‎ambazo hamna ushirikina wowote ndani yake, na hivyo kutabaruku na ‎maneno ya Mwenyezi Mungu.‎

Ama maandishi yoyote mengine, yasiyokuwa hayo ni haramu,, ‎kufuru na ushirikina. Na hayo ndiyo yale maandishi ya matalasimu ya ‎majina ya mashetani, majini, picha za mazingaumbwe mbali mbali, ‎michoro ya ramani, nyota, Mwezi, Jua,, na kadhalika, yote ni haramu, ‎kufuru, haijuzu hata kidogo. Ni talasimu za kishetani na kufuru. ‎Mwenyezi Mungu amesema: ‎

‏ وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ ‏السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ ‏فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ ‏وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا ‏بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ (البقرة 2 :102)

_‏Nawakafuata yale waliyoyazua mashetani kuuzulia Ufalme wa Sulaiman. ‎Na wala Sulaiman hakukufuru, bali mashetani ndio walio kufuru, ‎wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili, ‎Haatuta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha mtu ‎yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru! ‎Wakajifunza kutoka kwa hao wawili yale ya kumtenganisha mtu na mkewe. ‎Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa utashi wa Mwenyezi Mungu. Na ‎wanajifunza yanayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua ‎kwamba aliye chagua haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na ‎hakika ni uovu mno walio jiuzia nafsi zao; laiti wangelijua. (Al-Baqara, ‎‎2:102)‎_Na Mtume ‎ﷺ‎ amesema kuwa mazinguo ya talasimu za mashetani, na ‎Shanga, Tunguri na kadhalika ni ushirikina.‎

إن الرقى والتمائم والتولة شرك “. رواه أحمد و أبو داود
‎“Mazinguo ya mashetani, Kago na Tunguri ni ushirikina.” Ameipokea ‎Ahmad na Abu Daud.‎

B)‎ Kinga nyengine, ambazo si za maandishi, ni kinga zinazoaminiwa ‎kuhusiana na vitu mbali mbali, viwe venye roho au au visivyo na ‎roho, kwa imani ya kuwa vitu hivyo, vyenyewe, vinakulinda na ‎kukuhifadhi. Yaani itikadi potofu kuhusu vitu mbali mbali kuwa vina ‎nguvuza kukulinda jambo fulani, au kukupatia manufaa fulani. ‎Kinga za aina hii, kwa Kiarabu huitwa kwa majina mbali mbali, kama ‎Tamaaim, Tiwala, Khazar, Wada’, na kadhalika, ambazo kwa ‎Kiswahili ni sawa na maneno Kago, Ndumba, Tunguri, Ndonga, ‎Zindiko, Fingo, Hijabu, Azima na kadhalika, Kinga za aina hii ni ‎ushirikina na ukafiri uliokubuhu; maana ni kumtupilia mbali ‎Mwenyezi Mungu kama alivyesema:‎

ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ ثُمَّ إِذَا كَشَفَ الضُّرَّ عَنْكُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِنْكُمْ بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ ‏‏(النحل 16 : 54) ‏
Na anapo kuondosheeni madhara, mara kundi moja miongoni ‎mwenu, linamshirikisha Mola wao (An-Nahl, 16:54)‎

Na badala yake kugeukia kuamini kuwa Kago hizo zina nguvu ya ‎kuwalinda, kukuhifadhi na kuwakinga na jambo lolote lile wasilo litaka ‎liwafike, iwe kujikinga na maradhi, husuda, kijicho, shetani, jinni na ‎kadhalika, au viwanufaishe na jambo lolote lile, kama kukupa utajiri, ‎kwaharaka, biashara ichangamke, au kupasi mtihani na kadhalika. Ni ‎ushirikina. Vyote hivyo ni Shirk. Haramu. Kufuru. ‎
‎ ‎
Mtume ‎ﷺ‎ amesema kuhusu Talasimu na Kago kwa aina zake zote:‎

‏((من تعلق تميمة فلا أتم الله له، ومن تعلق ودعة فلا ودع الله له، ومن تعلق تميمة فقد أشرك))[رواه ‏‏ أحمد وغيره )‏
Ataye vaa kinga basi Mwenyezi Mungu asimkinge. Na atayejivesha hirizi ‎‎(tamiima) amemshirikisha Mwenyezi Mungu,” Ameipokea Ahmad na ‎wengine. ‎

عمران بن حصين “أن النبي صلى الله عليه وسلم أبصر على عضد رجل حلقة – قال: أراه قال: من ‏صفر -، فقال: ويحك ما هذه قال من الواهنة قال: أما إنها لا تزيدك إلا وهنا، انبذها عنك، فإنك لو ‏مت وهي عليك ما أفلحت أبدًا”2. ورواه ابن ماجة‏

Imepokewa kutoka kwa ‘Imraan bin Al-Huswayn ‎رضي الله عنه‎ ‎akisema: Mtume ‎ﷺ‎ alimuona mtu amejifunga kikuku mkononi- nadhani ‎cha shaba- akamuuliza: Ndiyo nini hiki? Akamibu kinaniondolea udhaifu. ‎Mtume ‎ﷺ‎ akamwambia: Kwa kweli hakikuzidishii kitu ila udhaifu tu. ‎Kivue ukitupilie mbali! Kwani lau kama utakufa na kikuku hicho kipo juu ‎ya mwili wako basi hutaweza kuokoka hata kidogo.” Ameipokea Ibn ‎Maja na Ahmad. ‎

عن عقبة بن عامر الجهني “أن رسول اللّه صلى الله عليه وسلم أقبل إليه رهط فبايع تسعة وأمسك ‏عن واحد. فقالوا: يا رسول اللّه، بايعت تسعة وأمسكت عن هذا؟ قال: إن عليه تميمة فأدخل يده ‏فقطعها، فبايعه. وقال: من علق تميمة فقد أشرك”.( رواه أحمد والحاكم )‏

Imepokewa kutoka kwa ‘Uqba bin ‘Amir al-Juhaniyy ‎رضي الله عنه‎ ‎akisema: Alikuwa Mtume ‎ﷺ‎ na kikundi cha watu 10. Basi akapokea Bay’a ‎‎(Ahadi ya Utiifu) kutoka kwa watu tisa, lakini akajizuwia kumpa mkono ‎mtu mmoja. Wale watu wakasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ‎umekubali Ahadi ya watu tisa, lakini umemkatalia huyu! Mtume ‎ﷺ‎ akasema: ‎Kwa sababu amevaa Kago. Basi yule mtu akaingiza mkono wake na ‎kuikata kamba ya ile Kago. Mtume ‎ﷺ‎ akampa mkono wa Bay’a, na kisha ‎akasema: Anayejivesha Kago amemshirikisha Mwenyuezi Mungu.” ‎Ameipokea Ahmad na Al-Hakim.‎

Naam, hakuna junaha ikiwa una maradhi maalumu, kama upungufu ‎wa madini fulani,, mwilini, na madaktari wakakuambia kuwa unahitaji ‎kuongeza madini fulani mwilini mwako, na wakapendekeza kutumia dawa ‎maalumu, au kuvaa kitu maalumu kitacho kusaidia kupata hayo madini ‎unayohitajia, basi hakuna junaha. Maana hapo una matatizo ya upungufu ‎wa kitu fulani mwilini mwako na madaktari wamekupa njia ya kujitibu. ‎Huko si kuamini kuwa hicho ulichovaa ndicho kinacho kusaidia, bali ni ‎kuamini kuwa umepewa dawa ya matatizo yako ya kiafya. Ni sawa na ‎kuandikiwa virutubisho fulani mwilini, kama Vitamin C. Hakuna junaha ‎hapo.‎

Kuna hadithi nyingi za kuharamisha kutumia vitu vyovyote vile kwa ‎imani kuwa vitu hivyo vyenyewe, ndio kinga, au hirizi inayo kulinda na ‎kukuhifadhi, au hata kukunufaisha kitu fulani. Miongoni mwa kago hizo, ‎za kishirikina, katika nchi zetu za Afrika ya Mashariki na kwengineko, ni ‎Makucha ya Simba, Kaure za pwani, Shanga, Mafupa ya wafu, Mafuvu ya ‎maiti, nywele za mkia wa simba au tembo, meno ya papa, au ya simba, ‎kucha za kima, meno ya sokwe, mafupa ya albino, ngozi ya albino, damu ‎ya hedhi (wanaita Limbwata), pembe za wanyama mbali mbali na ‎kadhalika. Vyote hivyo vinaingia katika jina la Kago, Ndunguri, Hijabu, ‎Pagao, Hirizi, Zindiko, Sihiri, Kinga, Fingo, Lindo na kadhalika na vyote ni ‎harmu, ushirikina na kufuru. Mwenye kuvaa ili vimlinde amekufuru. ‎Mwenye kuvitengeneza na kuwapa watu wavivae ili viwalinde amekufuru ‎maradufu. ‎

والله أعلم

وبالله التوفيق

السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم ‏

Imejbiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza ‎chchote, na kuweka kwenye FB yako au kwenye ‎WhatsApp na kwenye ‎Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *