KCWW 71\2 MLANGO WA UNYENYEKEVU NA UUNGWANA‎

Hadithi ya Marudio Jumapili, tarehe 17, Shaabani, 1446, sawa na 16 ‎Februari, 2025.‎‏‎ ‎

SEHEMU YA PILI.‎

KUHUSU FADHILA ZA UNYENYEKEVU NA UUNGWANA

‎71- Mlango wa unyenyekevu na uungwana kwa waumini.

Amesema Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالي‎ :- ‎

‎1.‎ Na wapokee kwa upole wale wanao kufuata miongoni mwa waumini ‎‎(Ash-Shu‘araa’: 215)‎

‎2.‎ Enyi mlio amini! Atakaye iacha Dini yake miongoni mwenu, basi ‎Mwenyezi Mungu Ataleta watu Anao wapenda, nao wanampenda, ‎wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri (Al-‎Ma’ida:54)‎

‎3.‎ Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na ‎mwanamke, na Tumekujaalieni muwe mataifa na makabila mbali ‎mbali ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi, miongoni mwenu, kwa ‎Mwenyezi Mungu, ni yule aliye mchamungu zaidi kati yenu (Al-‎Hujuraat:13)‎

‎4.‎ Basi msijisifu kuwa ni safi nafsi zenu; Yeye Anamjua sana mwenye ‎kujikinga na maovu (An-Najm:32)‎

‎5.‎ Na hao watu wa mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa ‎alama zao; Watasema: Ujima (umoja) wenu haujakusaidieni kitu, ‎na wala kiburi chenu. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa ‎Mwenyezi Mungu Hatawafikishia rehema? Ingieni Peponi, msiwe na ‎khofu, wala msihuzunike (Al-A‘raaf:48-49)‎

‎611. Imepokewa kutoka kwa al-Aswad bin Yaziid akisema: Aliulizwa ‎Bi. ‘Aisha ‎‏ رضي الله عنها‎ kitu gani alikuwa anakifanya nyumbani Mtume ‎‏ ﷺ‎? ‎Akasema: “Alikuwa anawahudumia wake zake, na Swala inaponadiwa, basi ‎hutoka kwenda kuswali.” Ameipokea Bukhari. ‎

‎612. Imepokewa kutoka kwa Abu Rifa’a Tamiim bin Usayd ‎رضي الله ‏عنه‎ akisema: nilifika kwa Mtume ‎‏ ﷺ‎ nikamkuta anahutubia watu, basi ‎nikasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Mgeni amekuja anauliza ‎kuhusu dini yake. Hajui kitu, kuhusu dini yake!” Akakatiza Mtume ‎ﷺ ‏‎ ‎hutuba yake, na kunijia nilipo. Akaekewa kiti, akakaa. Akaanza kunielimisha ‎alichoelimishwa na Mwenyezi Mungu. Alipomaliza akarudia kuhutubia ‎mpaka akamaliza.” Ameipokea Muslim. ‎

‎613. Imepokewa kutoka kwa Anas ‎رضي الله عنه‎ akisema: Alikuwa ‎Mtume ‎‏ ﷺ‎: anapomaliza kula chakula, huramba vidole vyake vitatu [gumba, ‎shahada na kidole cha kati]. Na alisema: ‎

‎“Ikidondoka tonge ya mmoja wenu, basi na aiokote, kisha aisafishe na aile; ‎kamwe asiiache kwa Shetani.” na ameamrisha kurambwa bakuli [sahani] na ‎kusema: “ Hamuwezi kujua, baraka ya chakula chenu iko wapi!” Ameipokea ‎Muslim.‎

‎614. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra ‎رضي الله عنه‎ akisema: ‎Amesema Mtume ‎‏ ﷺ‎: ‎

‎“Kila Mtume aliyepelekwa na Mwenyezi Mungu alichunga mbuzi.” ‎

Maswahaba wakamuuliza: “Hata wewe?” Akasema:“Ndiyo, hata mimi. ‎Nilikuwa nikiwachunga kwa ujira kutoka kwa wamiliki wake wa Makka.” ‎Ameipokea Bukhari. [Maridio ya Hadithi Nam.605.] ‎

‎615. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraya ‎رضي الله عنه‎ akisema: Amesema ‎Mtume ‎‏ ﷺ‎: “Lau kama nitaalikwa kwenda kula mguu au mkono wa mbuzi ‎nitaitika. Na lau kama nitazawadiwa mkono au mguu (au hata kwato) wa ‎mbuzi nitaupokea.” Ameipokea Bukhari. ‎

‎616. Imepokewa kutoka kwa Anas ‎رضي الله عنه‎ akisema: Alikuwa ‎Mtume ‎‏ ﷺ‎ na ngamia jike, anaitwa: al-‘Adh-baa’. Alikuwa ana kasi kubwa ‎sana; hawezekani kwa kukimbia, na karibu siku zote alikuwa anamshinda ‎mwenye kushindana naye. ‎

Siku moja, hata hivyo, akatokea bedui, akiwa amepanda kinda lake la ‎ngamia. Akashindana naye, akashindwa. Basi waislamu wakasikitishwa sana ‎na tukio hilo. Mtumeﷺ‎ akahisi kwamba wamesikitishwa kuona al-‘Adh-baa’ ‎ameshindwa. Basi akawapoza kwa kuwaambia:‎

‎“Msisikitishwe! Hivyo ndivyo Anavyofanya Mwenyezi Mungu; hakuna kitu ‎kitachopaa juu sana, duniani, ila kuna siku Mwenyezi Mungu Atakiteremsha ‎chini tu.” Ameipokea Bukhari. ‎

UFAFANUZI

Kuramba vidole, baada ya kula, na kabla ya kuosha mkono, ni Sunna. ‎Mtume ‎ﷺ‎ alikuwa akiramba vidole vyake vitatu, ambavyo ndivyo ‎alivyokuwa akilia chakula. Na hii inaonesha wazi wazi kuwa Mtume ‎ﷺ‎ ‎alikuwa akila vyakula vinavyoweza kuchukuliwa kwa vidole vitatu, kama ‎tende, mkate wa kuchovya kwenye “mchuzi” au kwenye supu, au nyama ya ‎kuchoma, na hivyo ni vidole hivyo vitatu ndivyo vilivyokuuwa vinaroa ‎chakula tepetepe, kama mchuzi. ‎

Hivyo basi, chakula chochote kile ambacho hakiwezi kuchotwa kwa vidole ‎vitatu, (kama wali na mchuzi, au ugali na mchuzi) basi kinaweza kuchotwa ‎kwa vidole zaidi ya vitatu, kama vidole vine, au hata vyote vitano; PASI NA ‎KUHUSISHA KIGANJA CHA MKONO. Haya ndiyo maadili ya kula chakula ‎kwa mkono. Mtume ‎ﷺ‎ , siku zote, alikuwa akichota chakula kwa vidole ‎vyake, tu, pasi na kuhusisha kiganja chake; tofauti na watu wengi, wenye ‎kupiga matonge makubwa kabisa, kwa kiganja chote cha mkono, ambalo ‎hawezi kulitia kinywaniu mpaka, kwanzaa, alikamue-kame na kulibinya-‎binya, ili liwe dogo la kuweza kuingizwa kinywani! Huo ni uroho na SI ‎sunna ya Mtume ‎ﷺ‎ . ‎

Kwa maana hiyo, mitindo yetu ya kuchota tonge kwa mkono wote, vidole ‎vitano na kiganja cha mkono, na kisha KUIVIRINGA VIRINGA TONGE, ‎ILI IWE NDOGO YA KUWEZA KUINGIA MDOMONI ni UROHO na ‎KARAHA na wala SI MAADILI YA KULA. Hakuna haja, wala si busara, ‎kuchota chakula kingi mkononi na kisha kukiminya minya ili kiweze kuingia ‎kinywani! NI UROHO NA SI JAMBO LA KUPENDEZA. Mtume ‎ﷺ‎ ‎hakupata kula kwa kuchanganya kiganja chake cha mkono kuchota chakula. ‎Siku zote kiganja chake cha mkono kilisalia kikavu. ‎

YALIYOMO NA YATOKANAYO

‎1.‎ Ukamilifu wa unyenyekevu wa Mtume ‎ﷺ‎ katika kuwahudumia wake ‎zake nyumbani.‎
‎2.‎ Sunna kwa Baba mzazi kusaidia kazi za nyumbani, kadiri ya uwezo ‎wake, na siyo kujigeuza mfalme Sulemani.‎

‎3.‎ Hima ya Mtume ‎ﷺ‎ kudumisha Swala katika wakati wake, na ‎kutokubali kushughulishwa na kitu chochote kengine, kufika hadi ‎kuchelewesha Swala katika wakati wake.‎

‎4.‎ Unyenyekevu wa Mtume ‎ﷺ‎ katika kuhudumia mambo ya Waislamu ‎wenye kuhitajia zaidi, msaada wake; kama alivyosita kuhutubia ili ‎kumfunza mpita njia aliyetaka aelimishwe kuhusu Dini yake, baadae ‎kurudi kuendelea kutoa hotuba yake. ‎

‎5.‎ Umuhimu wa kumjibu, kwa haraka iwezekanvyo, mwenye kuuliza ‎swali la Dini.‎

‎6.‎ Wanazuoni wamesema kuwa ni Wajibu kumshughulikia mtu aliyekuja ‎kuuliza kuhusu Imani na Dini yake, haraka iwezekanavyo na SI ‎KUAHIRISHA hadi avunjike moyo. Kama alivyofanya Mtume ‎ﷺ‎ na ‎mgeni huyu.‎

‎7.‎ Kujuzu kukatisha hotuba, hata kama hotuba ya Ijumaa, ikitokea ‎udhuru na dharura, na kisha kurudia kuondelea na hotuba.‎

‎8.‎ Kukatisha hotuba kwa kutembea hatua chache, au hata kukaa kitako, ‎kutokan na dharura, hakukatishi mfululilozo wa kisharia, hotuba ‎yenyewe. ‎

‎9.‎ Sunna ya kula kwa vidole vitatu: Kidole gumba, kidole cha Shahada ‎na kidole cha kaati.‎

‎10.‎ Karaha ya kula kwa mkono mzima, kuanzia vidole vitano hadi kiganja ‎cha mkono. Ni ishara ya uroho.‎

‎11.‎ Sunna ya kula kwa tonge ndogo ndogo, na si kwa MATONGE ‎MAKUBWA.‎

‎12.‎ Suna ya kuramba vidole, BAADA ya kumaliza kula, na kabla ya ‎kuosha mkono.‎

‎13.‎ Chakula kikidondoka na kikawa kinaweza kuokotwa na kusafishwa, ‎basi kiokotwe na kusafishwa na kisha kuliwa.‎

‎14.‎ Kisicho safishika kisiokotwe na kuliwa; lakini kinaweza kuokotwa na ‎kupewa wanyama wa kufugwa nyumbani, au hata wanayama wapita ‎njia.‎

‎15.‎ Sunna ya kuramba bakuli au sahani, baada ya kumaliza kula. Na ‎kuramba huku ni kwa vidole na SI KWA ULIMI, kama anavyo ramba ‎mbwa au paka.‎

‎16.‎ Kujuzu kwa waliokula kwa pamoja kuramba sahani au bakuli, kwa ‎vidole vyao na SI KWA NDIMI ZAO.‎

‎17.‎ Kila chakula kina baraka iliyofichwa na Mwenyezi Mungu katika ‎chakula hicho au chombo cha chakula hicho.‎

‎18.‎ Hima ya Uwislamu na mafunzo yake katika kuhifadhi na kulinda ‎neema za Mwenyezi Mungu.‎

‎19.‎ Uharamu wa kumwaga chakula, kwa kisingizio kuwa ni MAKOMBO.‎

‎20.‎ Uharamu wa kujaza chakula kwenye sahani, kupindukia uwezo wa ‎walaji kumaliza chakula kile, kiasi kwamba kinachosalia kinatupwa!‎

‎21.‎ Kuchunga n’gombe au mbuzi ni kazi ya Mitume, hivyo usimbeze ‎mchunga wanyama.‎

‎22.‎ Uhalali wa kupokea ujira kwa huduma halali uliyotoa.‎

‎23.‎ Wajibu wa kuitikia mwaliko wa chakula, hata kama ni supu ya miguu ‎ya mbuzi, isipokuwa kama una udhuru.‎

‎24.‎ Sunna ya kumualika nduguyo kwenye chakula na Wajibu wa kukubali ‎mwaliko huo; kwani jambo kama hilo ndilo linaloimarisha duguu na ‎mapenzi kati ya watu wawili.‎

‎25.‎ Kujuzu kufanya mashindano ya mbio na mfano wake: kama mbio za ‎riyadha, pasi na kucheza kamari. Kwani kamari ni HARAMU.\‎

‎26.‎ Kujuzu kumtunukia mshindi zawadi ya ushindi wake, ili kushajiisha ‎mashindano kama hayo ya halali, BILA YA ZAWADI HIYO ‎KUTOKANA NA KAMARI.‎

‎27.‎ Kila mshindi ana siku atashindwa; na kila kipandacho juu kuna siku ‎kitateremshwa chini. Hiyo ni KAWAIDA ya Mwenyezi Mungu kwa ‎viumbe vyake.‎

‎28.‎ Ukishindwa ukubali kushindwa, kwani hakuna kiumbe ambaye ‎atashinda siku zote. Kukataa kushindwa, unaposhindwa, ni KIRUBI, ‎hivyo ni HARAMU.‎

والله أعلم
‏ ‏
وبالله التوفيق‎ ‎

السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم.‏

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi ‎wa ‎Umma, ‎ambacho ni tafsiri kamili ya ‎رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ ‏مام ‏النووي ‏‎ ‎kilicho tungwa na Imam An-Nawawi na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili na ‎Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim ‎آل الشيخ ابى بكر بن ‏سالم‎.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako au kwenye ‎WhatsApp na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *