Hadithi za Marudio Jumamosi, tarehe 24 Mfungo Sita, 1446, sawa na 28 Septemba 2024.
KUHUSU KUWA NA MATUMAINI NA MWENYEZI MUNGU
SEHEMU YA SITA
51- Mlango wa Matumaini
Amesema Mwenyezi Munguسبحانه وتعالي :-
1. Na rehema Yangu imeenea kila kitu (Al-A‘raaf, 7: 156)
434. Imepokewa kutoka kwa Jabir رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Mfano wa Swala tano [kuziswali kila siku] ni mfano wa kuwepo mto wenye maji mengi, mbele ya mlango wa nyumba ya mmoja wenu, ambaye hukoga kwenye mto huo mara tano kila siku.”Ameipokea Muslim.
435. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbasرضي الله عنهما akisema: Nimemsikia Mtume ﷺ akisema: “Hatokufa Mwislamu akaswaliwa swala ya maiti na watu arubaini, wasio mshirikisha Allah na kitu chochote kile, isipokuwa Mwenyezi Mungu Atawakubalia dua zao njema wanazo muombea maiti huyo.”Ameipokea Muslim.
436.. Imepokewa kutoka kwa Ibn Mas‘udرضي الله عنه akisema: Tulikuwa kama watu arubaini, hivi, pamoja na Mtume ﷺ ndani ya kuba [hema la duara] akasema: “Je, mtaridhika mkiwa robo ya watu wa Peponi?’ Tukasema: “Ndiyo!” Akasema: “Je, mtaridhika mkiwa thuluthi moja ya watu wa Peponi?” Tukasema: “Ndiyo!” Akasema:
“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake! Mimi nataraji kuwa mtakuwa nusu ya watu wa Peponi; kwa sababu haingii mtu Peponi isipokuwa mwenye kuisalimisha nafsi yake kwa Mwenyezi Mungu. Na wingi wenu nyinyi, kulingana na wingi wa wale wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, ni kama wingi wa unyoya mweupe kwenye ngozi ya ng’ombe mweusi, au unyoya mweusi kwenye ngozi ya ng’ombe mwekundu.” Muttafaq ‘alayhi.
437. Imepokewa kutoka kwa Abu Musa al-Ash‘ariyyرضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Itapofika Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Atamkabidhi kila Mwislamu mmoja, Yahudi mmoja au Nasrani mmoja, na kumwambia: Huyu ni fidia yako ya kuokoka na Moto.”
Riwaya nyengine ya Abu Musa vile vile, inasema: “Amesema Mtume ﷺ: “Watakuja watu miongoni mwa Waislamu Siku ya Kiyama, wakiwa na madhambi mengi, mfano wa milima, lakini Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zao hizo.” Ameipokea Muslim.
Amesema Imam Nawawi: Maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu: “Huyu ni fidia yako ya kuokoka na Moto.” inaweza kueleweka zaidi kutokana na Hadithi nyengine, iliyopokelewa kutoka kwa Abu Hurayra, isemayo: “Kila mtu ana makaazi yake Peponi na makaazi mengine Motoni. Mwenye kuamini akiingia Peponi, basi makaazi yake ya Motoni huchukuliwa na kafiri; kwa sababu anastahiki makaazi hayo kwa ukafiri wake” Na maana ya “Fidia yako” ni kwamba: ulihatarika kuingia Motoni na huyu ndiye fidia yako; kwa sababu Mwenyezi Mungu Ameshatuwekea, tangu azali, idadi ya wataoujaza Moto. Hivyo, wakisha ingia makafiri Motoni, kwa kufuru zao, wanakuwa kama wamewafidia Waislamu nafasi zao Motoni. Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi!
438. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Umarرضي الله عنهما akisema: Nimemsikia Mtume ﷺ akisema: “Mwenye kuamini atasogezwa karibu na Mola wake, Siku ya Kiyama, mpaka afunikwe na rehema Zake, kisha Amhoji kwa madhambi yake; Atamwambia: “Unakumbuka dhambi fulani na dhambi fulani?” Atajibu: “Ndiyo Mola wangu! Nakumbuka.” Atamwambia: “Nilikusitiri nazo [nilikufichia] duniani, na leo Mimi Nakusamehe na kukufutia.” Basi atakabidhiwa ukurasa wa amali zake njema.” Hadithi zote hizi ni Muttafaq ‘alayhi
UFAFANUZI
Hadithi za sehemu hii zinaendelea kutufahamisha kuwa mwenye kumuamini, kwa dhati, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hapaswi kukata tamaa na Rehema za Mwenyezi Mungu, ilimradi tu anajitahidi kufanya amali njema, na kutaraji Rehema za Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwa amali njema muhimu kabisa ni Swala Tano za kila siku, ambazo anaye dumisha kuziswali, kila siku, hufutiwa dhambi zake zote kama alivyosema Mwenyezi Mungu :
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ (هود,11 : 114 )
“Na dumisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka.” (Huud, 11:114).
Hivyo, mfano wa kudumisha Swala tano kila siku, ni mfano wa mtu anayelazimika kuogelea, mara tano, kwenye maji mengi yaliyopo mbele ya nyumba yake, kila anapo toka au kurudi nyumbani, na hivyo kumfanya asafike na kila uchafu uliyopo juu ya mwili wake.
YALIYOMO NA YATOKANAYO
1. Umuhimu wa kudumisha Swala tano kila siku.
2. Kudumisha Swala tano kunapelekea kufutiwa madhambi yote madogo madogo.
3. Umuhimu wa Waumini walio hai kumuombea msamaha maiti Mwislamu.
4. Shafaa, kwa aliyekufa, ni KUMUOMBEA na SI KUMUOMBA maiti! Kumuomba maiti ni SHIRK!
5. Swala ya maiti ni muhimu sana na ni Ibada ya kumuombea maiti.
6. Umuhimu wa watu wengi sana kumswalia maiti; huenda pakapatikana, miongoni mwao, watu 40 au zaidi, wasiomshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, na ambao wakimuombea msamaha watakubaliwa.
7. Dua ya mja asiyemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote hairudi mikono mitupu. Hivyo, ukikutana na mcha Mungu (yuhai kama wewe) muombe akuombee dua!
8. Maombezi ya mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote hayakubaliwi.
9. Wingi wa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa waja Wake, ni sawa na WINGI wa manyoya ya ng’ombe mweusi, mwenye UNYOYA MMOJA MWEUPE, mwilini mwake!
10. Washirikina ni wengi sana kuliko Waumini halisi. Mwenyezi Mungu Amesema: وما أكثر الناس ولو حرصت بمؤمنين “Hata ufanye hima gani, bado wengi wa wanadamu si watu wenye kuamini (ni washirikina).
11. Dharura ya kuwa macho, kwa kila ulifanyalo, kuhakikisha HUMSHIRIKISHI Mwenyezi Mungu na kitu chochote kile: khasa katika KUOMBA!
12. Waja wengi wataoingia Peponi watatoka kwenye Umma wa Muhammad ﷺ .
13. Hatoingia Peponi ila mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu.
14. Bishara njema kwa Waumini wa Muhammad ﷺ
15. Pepo na Moto zimeshaumbwa na Mwenyezi Mungu na kila moja itakuwa na ujazo sawasawa wa idadi ya viumbe Vyake. (Yaani ukubwa wa kila moja unaweza kuchukua viumbe vyote alivyo viumba Mwenyezi Mungu)
16. Waliokufuru au kumshirikisha Mwenyezi Mungu, watatolewa kwenye nafasi za ujazo wao Peponi, na walio muamini wanachukua nafasi zao Peponi; vile nafasi za ujazo wao Motoni –kwa kumuamini Mwenyezi Mungu- zitachukuliwa na wale walionyimwa nafasi zao Peponi, kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu. [Ufafanuzi wa Imam Nawawi, ambao ni sahihi, unatokana na Hadithi Swahihi aliyoinukuu katika Ufafafnuzi wake, رحمه الله )
17. Dharura na umuhimu wa kuamini, na hatari na tahadhari ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote.
18. Fadhila za Mwenyezi Mungu kwa baadhi ya waja Wake, wenye kumuamini kwa dhati, ambao atawasitiri duniani na Akhera.
19. Kukiri kosa ni sawa na kuomba kufutiwa kosa ألإعتراف يمحو ألإقتراف.
20. Umuhimu wa kumsitiri Mwislamu kadiri iwezekanavyo.
21. Mlango wa Toba upo wazi na ni mpana sana.
وبالله التوفيق
الحقير إلى الله تعالى عبد القادر شريف آل الشيخ ابى بكر بن سالم
INAENDELEA…..
Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa Umma, ambacho ni tafisri kamili ya رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام النووي kilicho tungwa na Imam al-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na Sayyid Abdulqadir Shareef.
NI RUHUSA KUNUKUU NA kuweka kwenye FB yako au kwenye Whatsup na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com
Leave a Reply