KCWW. 51/7 MLANGO WA MATUMAINI

Hadithi za Marudio Jumapili, tarehe 25 Mfungo Sita, 1446, sawa ‎na 29 Septemba 2024.‎

KUHUSU KUWA NA MATUMAINI NA MWENYEI MUNGU

SEHEMU YA NANE NA YA MWISHO.‎

‎51- Mlango wa Matumaini

Amesema Mwenyezi Munguسبحانه وتعالي ‏‎ :-‎

Na rehema Yangu imeenea (imefunika) kila kitu (al-A’raaf: 156)‎

‎443. Imepokewa kutoka kwa Abu Nujayh, ‘Amr bin ‘Abasa –al-‎Sulamiyyرضي الله عنه ‏‎ akisema: Nilikuwa nikihisi, enzi za Ujahiliyya ‎‎[kabla ya Uwislamu] kwamba watu, kwa ujumla, wamepotea; hawafuati ‎haki hata kidogo kwani walikuwa wanaabudu masanamu. (Hadithi ndefu ‎kuhusu kusiliumu kwake Makka hadi kukutana tena na Mtume ‎ﷺ ‏Madina. ‎Anaendelea: ) ‎

Basi nikafunga safari kwenda Madina. Nilipofika nikamwendea na ‎kumwambia: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Unanikumbuka?” ‎Akasema: “Ndiyo! Wewe ndiye yule uliyekutana nami Makka.” ‎

Nikasema:“Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Nieleze kile ‎Alichokuelimisha Mwenyezi Mungu na ambacho mimi sikijui! Nielimishe ‎kuhusu Swala.” ‎

Akasema: “Swali swala ya asubuhi, na kisha jizuwiye kuswali ‎mpka baada ya kuchomoza Jua na kuinuka urefu wa mkuki – kwani, ‎wakati huo, huwa linachomoza baina ya pembe mbili za Shetani, na ‎wakati huo ndio makafiri wanalisujudia Jua. ‎

Baada ya hapo, unaweza kuswali, kwani swala wakati huo inatambuliwa ‎na huandikiwa thawabu yule mwenye kuiswali, mpaka kivuli cha mkuki ‎kilingane na urefu wake. Ifikapo wakati huo, jizuwiye kuswali; kwani ‎wakati huo ndio pale Moto wa Jahannam unapokolezwa kuni. Kivuli ‎kikipindukia zaid [ya urefu wa kivuli cha mkuki], unaweza kuswali; ‎kwani swala wakati huo inatambuliwa na huandikiwa thawabu yule ‎mwenye kuiswali hadi kuswali swala ya Asr. ‎

Baada ya Asri, jizuiye kuswali mpaka Jua lichwe, kwani linakuchwa ‎baina ya pembe mbili za Shetani, na wakati huo ndio makafiri ‎wanalisujudia.” ‎

Nikasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Nieleze kuhusu ‎udhu.” Akasema: ‎

‎“Yeyote yule anayejisogezea maji ya kutawadha, akasukutua, na kutema, ‎kisha akapandisha maji puani na kuyatoa, basi kwa kufanya hivyo, ‎makosa yote ya viungo vya uso wake, kinywa chake na pua yake ‎hupukutika na hutoweka, pamoja na maji hayo. ‎

Kisha akiosha uso wake, kama alivyo amrishwa na Mwenyezi Mungu, ‎basi makosa yote ya uso –kwa pande zote mbili za ndevu zake- ‎hupukutika na maji hayo. ‎

Kisha akiosha mikono yake mwili, hadi kwenye vifundo viwili, basi ‎makosa ya mikono yake hupukutika, pamoja na maji, kwenye ncha za ‎vidole vake. ‎

Kisha akipangusa kichwa chake, basi makosa ya kichwa chake ‎hupukutika, na maji, kwenye ncha za nwele zake. ‎

Kisha akiosha miguu yake miwili hadi kwenye vifundo viwili vya miguu, ‎basi makosa ya miguu yake hupukutika, pamoja na maji, kupitia ncha za ‎vidole vyake. ‎

Akisimama akaswali, akamshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu na ‎kumtukuza kama Anavyo stahiki kusifiwa na kutukuzwa, na akaelekeza ‎moyo wake wote kwa Mwenyezi Mungu, basi makosa yake yote ‎hutoweka na kuwa hana makosa kabisa, kama siku aliyozaliwa na mama ‎yake.”‎

Basi ‘Amr bin ‘Abasa akamsimulia Hadithi hii Abu Umama –‎swahaba wa Mtume ‎ﷺ ‏‎. Abu Umama akamwambia ‘Amr: “Ewe ‘Amr! ‎Tahadhari na unayosema! Mtu anapewa malipo yote hayo uliyotaja ‎mahali pamoja!” ‎

‎‘Amr akamjibu: “Ewe Abu Umama! Mimi nimesha zeeka, mifupa yangu ‎imeshadhoofika, mauti yananisogelea, na sina haja kumsingizia ‎Mwenyezi Mungu wala Mjumbe Wake! Lau ningekuwa sikumsikia ‎Mtume ‎ﷺ ‏akisema maneno hayo, si mara moja, si mara mbili, si mara tatu ‎‎(akahisabu mpaka saba) basi nisingeliyasimulia kamwe. Lakini, ukweli ni ‎kwamba nimemsikia akisimulia mara nyingi sana.” Ameipokea Muslim. ‎‎[Angalia pia Hadithi Nan.131]‎

Amesema Imam Nawawi: Maneno ya Mtume ‎ﷺ ‏‎: “Baina ya pembe ‎mbili za Shetani.” yaani kuelekea kwenye kichwa chake, na ni mfano wa ‎kumaanisha kuwa wakati huo ndio wakati ambao Shetani na wafuasi ‎wake wanafanya vitimbi vyao vya kufuru na kutaka kuwashirikisha ‎wengine.” ‎

‎444. Imepokewa kutoka kwa Abu Musa al-Ash’ariyy ‎رضي الله عنه ‏akisema: Amesema Mtume ‎ﷺ ‏‎ ‎

‎“Akiutakia kheri umma Mwenyezi Mungu, basi humchukua Mtume wao ‎kabla ya wao, na kumfanya awe mtayarishaji wao wa mambo mazuri, na ‎pia hazina yao Siku ya Kiyama. ‎

Na akiutakia shari umma basi huuangamiza vile Mtume wao yungali hai; ‎akiona kwa macho yake jinsi wanavyo angamizwa. Na huko ni ‎kumliwaza kwa walivyo mkadhibisha na kukataa kufuata maamrisho ‎yake kwao.” Ameipokea Muslim.‎

UFAFANUZI.‎

Hadithi hizi mbili na Aya iliyotangulia, zinatuhitimishia maudhui ya ‎mlango huu, ya kuwa na matumaini mema na Mwenyezi Mungu. Kwani ‎Kutawadha udhu kamilifu, na kuswali rakaa mbili kwa utulivu na – sunna ‎ya baada ya kutawadha- kunatosha kuwa ndio sababu ya kufutiwa ‎dhambi zote –isipokuwa dhambi kubwa kubwa ‎الكبائر ‏‎. ‎

Na itoshe, kwetu sisi, kushukuru kwamba Umma huu, ambao sisi tumo, ‎tumerehemewa na Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالى ‏‎ kwa kumchukua ‎Mtume Wake na kutuacha sisi tumfuatie mmoja mmoja, ili atutangulie ‎mbele ya Mwenyezi Mungu. Hiyo, peke yake, inatosha kutupa matumaini ‎makubwa kwa Mola wetu.‎

YALIYOMO NA YATOKANAYO.‎

‎1.‎ Fadhila za Udhu na fadhila za rakaa mbili za sunna ya Udhu.‎
‎2.‎ Umuhimu wa kutawadha kikamilifu na kuswali kwa unyenyekevu.‎
‎3.‎ Inakatazwa kuswali baada ya Swala ya Alfajiri, wakati wa ‎kuchomoza Jua, hadi liinuke kadiri ya urefu wa mkuki.‎
‎4.‎ Inakatazwa kuswali baada ya Swala ya Laasiri na wakati Jua ‎linakuchwa. ‎
‎5.‎ Nyakati hizi mbili ni vibaya –yaani makuruhu- kuswali swala ‎yoyote, pasi na dharura.‎
‎6.‎ Fadhila za Kuswali Swala ya Dhuha, na wakati wake ni tokea ‎baada ya Jua kuinuka urefu wa mkuki, hadi majira ya Swala ya ‎Adhuhuri –i.e. kivuli cha urefu wa mkuki kuwa sawa na urefu wa ‎mkuki weneywe, upande wa magharibi-. ‎
‎7.‎ Fadhila za Sunna baada ya Adhuhuri na kabla ya kuswali Swala ya ‎Laasiri. Kwani wakati huo, hata malaika huswali pamoja, na ‎kushuhudia Sunna zako.‎
‎8.‎ Wajibu na Umuhimu wa unyenyekevu katika Ibada.‎
‎9.‎ Ukosefu wa unyenyekevu, katika ibada, unapunguza thawabu za ‎ibada hiyo.‎
‎10.‎ Fadhila na Umuhimu wa Mwislamu kuwa na matumaini mema na ‎Mwenyezi Mungu.‎
‎11.‎ Kuwa na matumaini na Mwenyezi Mungu ni kutenda mema na SI ‎kubweteka.‎
‎12.‎ Kubweteka na kujipa matumaini kwa Mwenyezi Mungu ni ‎kujidanganya.‎
‎13.‎ Kutawakali ni kumuamini Mwenyezi Mungu na kutenda ya ‎aliyokuamrisha kuyatenda.‎
‎14.‎ Fadhila za Abu Nujayhi ‎رضي الله عنه ‏
‎15.‎ Uangavu, umakini na ukali wa ubongo wa Mtume ‎ﷺ‎ kumtambua ‎mtu, aliyekutana naye, zaidi ya miaka 10 iliyopita!‎
‎16.‎ Hima, hekima na busara ya Mtume ‎ﷺ‎ katika kuongoza na ‎kuelimisha Maswahaba wake.‎
‎17.‎ Umma wa Muhammad ‎ﷺ ‏‎ umebahatika kwa kutopatilizwa, kabla ‎ya yeye kuitikia Wito wa Mola wake.‎
‎18.‎ Kutangulia kwa Mtume, yeyote yule, kwenda kwa Mola wake ni ‎rehema kwa Umma wake.‎
‎19.‎ Watu walioangamizwa kabla ya vifo vya Mitume wao, ‎wamelaaniwa na kutengwa na Rehema za Mwenyezi Mungu.‎
‎20.‎ Hatari ya kwenda kinyume na mafundisho na mafunzo ya Mtume ‎Muhammad ‎‏’ﷺ ‏‎; kwani hakuna usalama kwa kufanya hivyo.‎
‎21.‎ Uokofu ni kufuata aliyokuja nayo Bwana wetu, Muhammad ‎ﷺ‎ , tu.‎

والله أعلم
‏ ‏
وبالله التوفيق‎ ‎

السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم.‏

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi ‎wa ‎Umma, ‎ambacho ni tafsiri kamili ya ‎رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ ‏مام ‏النووي ‏‎ ‎kilicho tungwa na Imam An-Nawawi na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili ‎na Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim ‎آل الشيخ ابى ‏بكر بن سالم‎.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako au kwenye ‎WhatsApp na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *