KCWW. 51/5 MLANGO WA MATUMAINI

Hadithi za Marudio Jumapili, tarehe 18 Mfungo Sita, 1446, sawa ‎na 22 Septemba 2024.‎

KUHUSU KUWA NA MATUMAINI NA MWENYEZI MUNGU

SEHEMU YA TANO.‎

‎51- Mlango wa Matumaini

Amesema Mwenyezi Munguسبحانه وتعالي ‏‎ :-‎

‎5.‎ Na rehema Yangu imeenea (imefunika) kila kitu (Al-A‘raaf, ‎‎7:156)‎

‎430. Imepokewa kutoka kwa ‘Abdullah bin ‘Amr bin al-‘As‎رضي ‏الله عنهما ‏‎ akisema: Alisoma Mtume ‎ﷺ ‏‎ maneno ya Mwenyezi Mungu, ‎yenye kusimulia dua ya Nabii Ibrahim ‎عليه السلام ‏‎ Ewe Mola wangu Mlezi! ‎Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi aliye nifuata mimi huyo ni ‎wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe, Mwenye ‎kurehemu (Ibrahim:36) na maneno ya Mwenyezi Mungu, yenye ‎kusimulia dua ya Nabii ‘Isa ‎عليه السلام ‏‎ : Ukiwaadhibu basi wao ni waja ‎Wako, na ukiwasamehe basi hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye ‎hekima (Al-Ma’ida, 5:118) alipomaliza kusoma, aliinua mikono yake juu ‎na kusema: ‎
‎“Ewe Mola wangu! Umma wangu, Umma wangu!” kisha akalia! ‎

Mwenyezi Mungu akamtuma Jibril na kumuagiza kwa ‎kumwambia: “Jibril! Nenda kwa Muhammad ukamuulize–na Mola wako ‎Anajua zaidi- kinamliza nini?” ‎

Basi Jibril akamuendea na kumuuliza. Na Mjumbe wa Mwenyezi ‎Mungu akamjibu – na Mwenyezi Mungu Anakijua- kile alichokisema. ‎Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Jibril: ‎

‎“Ewe Jibril! Nenda kwa Muhammad na mwambie: “Tutakuridhisha kwa ‎Umma wako na wala Hatutakuhuzunisha!” Ameipokea Muslim. ‎

‎431. Imepokewa kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal ‎رضي الله عنه ‏‎ ‎akisema: Alinipakia Mtume ‎ﷺ ‏‎ juu ya punda wake, akaniita kwa kusema: ‎
‎“Ewe Mu‘adh! Unajua nini haki ya Mwenyezi Mungu juu ya waja Wake? ‎Na nini haki ya waja wa Mwenyezi Mungu, kwa Mola wao?” Nikajibu: ‎‎“Mwnyezi Mungu na Mutme Wake ndio wanao jua zaidi.” Akasema: ‎

‎“Haki ya Allah kwa waja wake ni kumuabudu Yeye peke Yake, ‎pasi na kumshirikisha na chochote. Na haki ya waja kwa Mwenyezi ‎Mungu ni kutomuadhibu yeyote yule ambaye hamshirikishi na kitu ‎chochote!” ‎

Nikasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Je, unaniruhusu ‎niwabashirie watu habari hiyo!” Akasema: “Hapana, usiwabashirie; ‎watabweteka!” Muttafaq ‘alayhi. [Angalia pia Hadithi Nam.420, mlango ‎huu huu]‎

‎432. Imepokewa kutoka kwa al-Bara’ bin ‘Azibرضي الله عنهما ‏‎ ‎akisema: Amesema Mtume ‎ﷺ ‏‎: “Mwislamu ataposailiwa [hojiwa] ‎kaburini, atajibu kuwa anashuhudia kwamba hapana mola wa kuabudiwa ‎kwa kweli ila Allah na Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na ‎hiyo ndiyo maana ya Maneno ya Mwenyezi Mungu: Mwenyzi Mungu ‎Huwathibitisha [huwawezesha] wenye kuamini kwa kauli sahihi, katika ‎maisha ya dunia na ya Akhera (Ibrahim: 27) Muttafaq ‘alayhi. ‎

‎433. Imepokewa kutoka kwa Anas ‎رضي الله عنه ‏‎ akisema: Amesema ‎Mtume ‎ﷺ ‏‎: “Pale kafiri anapofanya jambo moja jema basi hulipwa, kwa ‎jema hilo, malipo ya kidunia [hapa hapa duniani]. Lakini mwenye ‎kuamini, huekezewa katika amali zake njema Siku ya Akhera, na hupewa ‎riziki duniani, kwa utiifu wake.”‎

Riwaya nyengine, ya Muslim, inasema: “Mwenyezi Mungu ‎Hamdhulumu (Hamnyimi) – mwenye kuamini- jema lolote lile alifanyalo; ‎maana hulipwa kwa riziki duniani, na Akhera hulipwa kwa thawabu. ‎Ama kafiri, yeye hulipwa riziki, duniani, kwa mema anayofanya kwa ajili ‎ya Mwenyezi Mungu, lakini akifika Akhera hana kitu chema cha ‎kulipwa.” Ameipokea Muslim.‎

UFAFANUZI

Bado tumo katika mlango wa kutokata tamaa na umuhimu wa kuwa na ‎Matumaini mema kwa Mwenyezi Mungu, ilimradi Matumaini mema hayo ‎yatokane na Imani thabiti, na yafuatiwe na kuomba msamaha kwa wingi, ‎na kutubu kwa kauli na vitendo. Kutumaini Rehema za Mwenyezi Mungu ‎pasi na kumuamini ni sawa na kutaraji kunywa maji kutoka kwenye jiwe ‎manga (sulubu\gumu) Au kutaraji kupata gudulia la maji baridi Motoni!‎

Hivyo, Imani, Istighfaar na Tawba, kwa kauli na vitendo ndio chanzo na ‎ufunguo wa kutokata tamaa. Bali ndio shahada ya kupata Radhi za ‎Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالى ‏‎; maana Imani ni Kauli na Vitendo. Kama ‎ilivyo Ukafiri ni kauli na vitendo. ‎

YALIYOMO NA YATOKANAYO

‎1.‎ Mwenye kumuamini Allah na Mtume Wake, kamwe hakati tamaa ‎na Mwenyezi Mungu.‎
‎2.‎ Shafaa=maombezi ya Mtumeﷺ ‏‎ , Siku ya Kiyama, yanamjumuisha ‎kila aliyemuamini na kumfuata.‎
‎3.‎ Hadithi hii, ni miongoni mwa Dalili kubwa, za kuweko Shafaa ya ‎Mtume ‎ﷺ ‏‎ Siku ya Kiyama, kwa waliomuamini na kumfuata.‎
‎4.‎ Ukubwa na Wingi wa huruma za Mtume ‎ﷺ ‏‎ kwa umma wake.‎
‎5.‎ Ukubwa na Wingi wa Mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume ‎Wake, Muhammad ‎ﷺ ‏
‎6.‎ Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu anapendwa Naye kiasi hicho, ‎iweje sisi tusiweze kumpenda na kumtukuza anavyostahiki ‎kupendwa na kutukuzwa!‎
‎7.‎ Kumpenda Mtume ‎ﷺ ‏‎ ni WAJIBU juu yetu, na ni budi kumpenda ‎zaidi ya kiumbe yeyote mwengine, zaidi kuliko mali zetu, watoto ‎wetu, bali hata nafsi zetu:- ‎لايؤمن عبد حتى أكون أحب إليه من ولده ووالده ‏والناس أجمعين (رواه مسلم -44 – وغيره)‏
‎8.‎ Kumuabudu Mwenyezi Mungu, Pekee, pasi na kumshirikisha na ‎chochote kile ni WAJIBU MTAKATIFU wa kila mja, na ‎atayefanya hivyo kwa dhati ni budi kuingia Peponi.‎
‎9.‎ Mwenyezi Mungu Ametoa dhamana – kutokana na Fadhila Zake ‎na Ukarimu Wake- kutomuingiza Motoni, yeyote yule atayetimiza ‎WAJIBU wake MTAKATIFU wa kumuabudu, Pekee, pasi na ‎kumsirikisha na chochote kile.‎
‎10.‎ Kuhakikishiwa Matumaini mema hakumaanishi ubweteke tu; ‎kwani kila mtu hufanyiwa wepesi kutenda liliyomo katika masjala ‎yake, isipokuwa akiomba asaidiwe. ‎لايرد القضاء إلا الدعاء ‏‎ Ni Dua ‎pekee ndiyo inayoweza kubadilisha au kufuta yaliyoandikwa ‎kwenye masjala. ‎
‎11.‎ Hatari ya kumsirikisha Allah na kitu chochote kile, iwe katika ‎kumuabudu, katika Majina Yake, Sifa Zake, kutii Amri Zake, na ‎kadhalika: ‎مخلصين له الدين ‏‎= kwa Kumtakasia Ibada kikamilifu. ‎HAKUNA MCHEZO KATIKA HILI!‎
‎12.‎ Kusailiwa kaburini, mara, tu, baada ya kuzikwa, ni Haki. Na ‎hakuna mtu atayeweza kubadilisha, au kubadilishiwa majibu yake, ‎isipokuwa amali zake alizozitenda Duniani. ‎
‎13.‎ Ni Mwenyezi Mungu, pekee, ndiye Mwenye kumpa Kauli Thaabit, ‎kaburini, yule aliyemuamini; na SI ‎تلقين ‏‎ :IMLA(dictation) ya walio ‎hai! Na hiyo ndiyo maana ya Aya ya 27 ya Surat Ibrahim.‎
‎14.‎ Umuhimu wa kumuombea maiti, kwa Mwenyezi Mungu, Ampe ‎kauli thabit, na SI UFIDHULI wa kumfundisha aseme nini! ‎Munkar!‎
‎15.‎ Ni amali za mja, alizotenda duniani, ndizo zitazomsaidia au ‎kumtosa baada ya kufa. ‎
‎16.‎ ‎ Maiti anaombewa haombwi! Akiombwa ameshirikishwa na ‎Mwenyezi Mungu!‎
‎17.‎ Hakuna amali isiyo na malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu! ‎Wema kwa wema na uovu kwa uovu.‎
‎18.‎ Wema wa kafiri duniani hulipwa hapa hapa duniani; akienda ‎Akhera hana lake ila amali za ukafiri wake.‎
‎19.‎ Ukafiri unafuta malipo ya amali njema Akhera.‎
‎20.‎ Wema wa Muumini hulipwa duniani na Akhera, au huekezewa ili ‎alipwe vyema zaidi Akhera. Duniani hurahisishiwa rizki yake kwa ‎utiifu wake.‎
‎21.‎ Imani haifuti, bali inaweza kuchelewesha tu, malipo mema, hapa ‎duniani, lakini ni budi kulipwa mema, Akhera.‎
‎22.‎ Kipimo na Kigezo cha kukubaliwa au kukataliwa Amali za ‎Mwanadamu ni Imani sahihi na utakaso wa Nia.‎
‎23.‎ Ewe Mwenye kuamini! Usikate tamaa kutokana na Rehema za ‎Allah!‎

وبالله التوفيق ‏

الحقيرإلى الله تعالى عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكربن سالم

INAENDELEA… ‎

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa ‎Umma, ambacho ni tafisri kamili ya ‎رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام ‏النووي ‏kilicho tungwa na Imam al-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na ‎Sayyid Abdulqadir Shareef.‎
NI RUHUSA KUNUKUU NA kuweka kwenye FB yako au kwenye ‎Whatsup na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa ‎lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie ‎thawabu.‎
kcwajawema@gmail.com

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *