DARSA YA BM.14.4\3 MLANGO WA UDH-HIYA

Hadithi ya Leo, Alhamisi, tarehe 29, Rajab, 1446, sawa na tarehe 30, JANUARI, 2025

KUHUSU KUCHINJA MNYAMA WA UDH-HIYA

SEHEMU YA TATU

1348 – وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ  {“مَنْ كَانَ لَهُ سَعَةٌ وَلَمْ يُضَحِّ، فَلَا يَقْرَبَنَّ مُصَلَّانَا” } رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَابْنُ مَاجَه، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ، لَكِنْ رَجَّحَ اَلْأَئِمَّةُ غَيْرُهُ وَقْفَه.

  1. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه akisema: “Amesema Mtume : “Mwenye uwezo na wasaa wa kuchinja mbuzi wa Udh-hiya halafu asichinje, asije kuswali nasi Swala ya Idi.” Ameipokea Ahmad na Ibn Majah na ameisahihisha Al Hakim. Baadhi ya wanazuoni wa Hadithi, hata hivyo, wamesema Hadithi hii haitoki moja kwa moja kutoka kwa Mtume, ﷺ, bali ni maneno ya Swahaba. [Ila hawezi Abu Hurayra kusema maneno hayo kutoka kichwani mwake tu, lazima amemsikia Mtume ﷺ akisema!]

UFAFANUZI

Hadithi hii inatuzindua na kututanabahisha kuwa kuchinja mnyama wa Udh-hiya ni Ibada kubwa sana kwa mwenye uwezo na wasaa wa kutekeleza Ibada hiyo asubuhi ya Sikukuu ya Mfungo Tatu. Hivyo, mtu yeyote mwenye uwezo na nafsi ya kuchija mnyama wa Udh-hiya, lakini akapuuza kwa makusudi au akaacha kuchinja, basi ni bora asiende kuswali Swala ya Idi, na Waislamu wengine waliokwisha fanya Ibada hiyo, kabla ya kwenda panapo swaliwa Swala ya Idi.  Hilo ni onyo kali kabisa kuhusu kudharau au kupuuza kuchinja mnyama wa Udh-hiya, licha ya kwamba mhusika ana uwezo wa fedha na nafasi ya kufanya hivyo. Kwa maneno mengine, kuchinja mnyama wa Udh-hiya, asubuhi ya Sikukuu ya Mfungo tatu, ni ibada kubwa sana ya kujitolea. Mtu pekee anayesamehewa ni asiyekuwa na uwezo wa hali wala mali, kufanya Ibada hiyo; kama mtoto mdogo, au mwenda wazimu. Ni kutokana na maana ya Hadithi hii, ndiyo maana Imam Abu Hanifa akachukua msimamo wa Wajibu kuchinja mnyama wa Udh-hiya. Maimamu wengine, hata hivyo, wamechukua msimamo wa kuwa Kuchinja mnyama wa Udh-Hiya ni Sunna, si wajibu.  Miongoni mwa dalili zao, ni Hadithi nyingi, ila itoshe kunukuu Hadithi moja tu, isemayo:

عن ابن عباس: أن النبي -صلى الله عليه وسلم- قال: “ثلاثٌ هي عليَّ فرائض، ولكم تطوع: النحر، والوتر، وركعتا الفجر”. أخرجه الدارقطني (2/ 21)، والحاكم (1/ 441)
Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbas رضي الله عنهما akisema: “Amesema Mtume ﷺ : Mambo matatu kwangu mimi ni Faradhi, lakini kwenu nyinyi ni Sunna za kujitolea. 1.Kuchinja mnyama wa Udh-hiya, 2. Swala ya Wittri, na 3. Rakaa mbili kabla ya Swala ya Al-Fajiri.” Ameipokea Daraqutniyy, H.2/21, na Al-Hakim, H.1/441.
Hivyo, kuchinja mnyama wa Udh-hiya, asubuhi ya Sikukuu ya Mfungo Tatu, iwe kabla au baad ya Swala ya Idi, ni Sunna kubwa sana, kwa mwenye uwezo wa hali na mali.

YALIYOMO NA YATOKANAYO

  1. Kuchinja mnyama wa Udh-hiya asubuhi ya Sikukuu ya Mfungo tatu ni Sunna kubwa sana, iliyotiliwa mkiazo kwa mwenye uwezo wa hali na mali.
  2. Mwenye uwezo wa hali na mali, kuchinja mnyama wa Udh-hiya, kisha akapuuza kuchinja, hana sababu ya kwenda kuchanganyika na Waislamu kuswali swala ya Idi husika.
  3. Swala ya Idil Adh-ha, inafuatilia Ibada ya Kuchunha mnyama wa Udh-hiyo; hivyo atayechinja mnyama wa Udh-hiya, baada ya Sala ya Idi, atakuwa ametekeleza, sawa sawa, Ibada hiyo. Lakini akichinja Kabla ya Swala ya Idi, atakuwa hajafuata Sunna ya Mtume ﷺ , ila Udh-hiya yake imesihi.
  4. Asiye na uwezo wa hali wala wa mali hakalifishwi kuchinja mnyama wa Udh-hiya, bali anakuwa miongoni wa wenye kugaiwa nyama ya Udh-hiya.

والله أعلم

وبالله التوفيق

HIFADHI NDANI YA SIMU YAKO ILI UWEZE KUMTUMIA MWENZAKO!‎ ‎
IMETAYARISHWA na Sayyid Abdulqadir Shareef
*Mtumishi wa Sunna za Mtume ﷺ *

من السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
خادم السنة النبوية

KUTOKA KITABU CHA بلوغ المرام من أدلة الأحكام UFIKIAJI WA MALENGO KUPITIA HADITHI ZA FIQHI YA MILANGO*

JIUNGE NA KUMBI ZA DARSA ZA SAYYID ABDULQADIR SHAREEF, KWA KUTUMA MAOMBI YAKO, MOJA KWA MOJA, KWENDA NAMBA +255786887887, KUPITIA WHATSAP
LAZIMA UTAJE MAJINA YAKO HALISI MATATU NA MAHALI ULIPO! SHARIA ZA MITANDAO TANZANIA

UKIWA NA SUALA LOLOTE, LINALOKUHUSU WEWE MWENYEWE, NA SI KUMHUSU MTU MWENGINE, USIMTUMIE MWENYE KUTOA DARSA, BALI MTUMIE ADMIN WA UKUMBI WAKO, AKUPATIE JIBU, KAMA LIPO JIBU LAKE, KUTOKANA NA MAJIBU ZAIDI YA 3000, AU ALIWEKE SUALA LAKO KUMBINI, LISUBIRI KUJIBIWA! USIMTUMIEA MTOA DARSA.

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *