Hadithi ya Marudio Jumapili, tarehe 17, Shaabani, 1446, sawa na 16 Februari, 2025.
SEHEMU YA PILI.
KUHUSU FADHILA ZA UNYENYEKEVU NA UUNGWANA
71- Mlango wa unyenyekevu na uungwana kwa waumini.
Amesema Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالي :-
1. Na wapokee kwa upole wale wanao kufuata miongoni mwa waumini (Ash-Shu‘araa’: 215)
2. Enyi mlio amini! Atakaye iacha Dini yake miongoni mwenu, basi Mwenyezi Mungu Ataleta watu Anao wapenda, nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri (Al-Ma’ida:54)
3. Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke, na Tumekujaalieni muwe mataifa na makabila mbali mbali ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi, miongoni mwenu, kwa Mwenyezi Mungu, ni yule aliye mchamungu zaidi kati yenu (Al-Hujuraat:13)
4. Basi msijisifu kuwa ni safi nafsi zenu; Yeye Anamjua sana mwenye kujikinga na maovu (An-Najm:32)
5. Na hao watu wa mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa alama zao; Watasema: Ujima (umoja) wenu haujakusaidieni kitu, na wala kiburi chenu. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi Mungu Hatawafikishia rehema? Ingieni Peponi, msiwe na khofu, wala msihuzunike (Al-A‘raaf:48-49)
611. Imepokewa kutoka kwa al-Aswad bin Yaziid akisema: Aliulizwa Bi. ‘Aisha رضي الله عنها kitu gani alikuwa anakifanya nyumbani Mtume ﷺ? Akasema: “Alikuwa anawahudumia wake zake, na Swala inaponadiwa, basi hutoka kwenda kuswali.” Ameipokea Bukhari.
612. Imepokewa kutoka kwa Abu Rifa’a Tamiim bin Usayd رضي الله عنه akisema: nilifika kwa Mtume ﷺ nikamkuta anahutubia watu, basi nikasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Mgeni amekuja anauliza kuhusu dini yake. Hajui kitu, kuhusu dini yake!” Akakatiza Mtume ﷺ hutuba yake, na kunijia nilipo. Akaekewa kiti, akakaa. Akaanza kunielimisha alichoelimishwa na Mwenyezi Mungu. Alipomaliza akarudia kuhutubia mpaka akamaliza.” Ameipokea Muslim.
613. Imepokewa kutoka kwa Anas رضي الله عنه akisema: Alikuwa Mtume ﷺ: anapomaliza kula chakula, huramba vidole vyake vitatu [gumba, shahada na kidole cha kati]. Na alisema:
“Ikidondoka tonge ya mmoja wenu, basi na aiokote, kisha aisafishe na aile; kamwe asiiache kwa Shetani.” na ameamrisha kurambwa bakuli [sahani] na kusema: “ Hamuwezi kujua, baraka ya chakula chenu iko wapi!” Ameipokea Muslim.
614. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ:
“Kila Mtume aliyepelekwa na Mwenyezi Mungu alichunga mbuzi.”
Maswahaba wakamuuliza: “Hata wewe?” Akasema:“Ndiyo, hata mimi. Nilikuwa nikiwachunga kwa ujira kutoka kwa wamiliki wake wa Makka.” Ameipokea Bukhari. [Maridio ya Hadithi Nam.605.]
615. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraya رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ: “Lau kama nitaalikwa kwenda kula mguu au mkono wa mbuzi nitaitika. Na lau kama nitazawadiwa mkono au mguu (au hata kwato) wa mbuzi nitaupokea.” Ameipokea Bukhari.
616. Imepokewa kutoka kwa Anas رضي الله عنه akisema: Alikuwa Mtume ﷺ na ngamia jike, anaitwa: al-‘Adh-baa’. Alikuwa ana kasi kubwa sana; hawezekani kwa kukimbia, na karibu siku zote alikuwa anamshinda mwenye kushindana naye.
Siku moja, hata hivyo, akatokea bedui, akiwa amepanda kinda lake la ngamia. Akashindana naye, akashindwa. Basi waislamu wakasikitishwa sana na tukio hilo. Mtumeﷺ akahisi kwamba wamesikitishwa kuona al-‘Adh-baa’ ameshindwa. Basi akawapoza kwa kuwaambia:
“Msisikitishwe! Hivyo ndivyo Anavyofanya Mwenyezi Mungu; hakuna kitu kitachopaa juu sana, duniani, ila kuna siku Mwenyezi Mungu Atakiteremsha chini tu.” Ameipokea Bukhari.
UFAFANUZI
Kuramba vidole, baada ya kula, na kabla ya kuosha mkono, ni Sunna. Mtume ﷺ alikuwa akiramba vidole vyake vitatu, ambavyo ndivyo alivyokuwa akilia chakula. Na hii inaonesha wazi wazi kuwa Mtume ﷺ alikuwa akila vyakula vinavyoweza kuchukuliwa kwa vidole vitatu, kama tende, mkate wa kuchovya kwenye “mchuzi” au kwenye supu, au nyama ya kuchoma, na hivyo ni vidole hivyo vitatu ndivyo vilivyokuuwa vinaroa chakula tepetepe, kama mchuzi.
Hivyo basi, chakula chochote kile ambacho hakiwezi kuchotwa kwa vidole vitatu, (kama wali na mchuzi, au ugali na mchuzi) basi kinaweza kuchotwa kwa vidole zaidi ya vitatu, kama vidole vine, au hata vyote vitano; PASI NA KUHUSISHA KIGANJA CHA MKONO. Haya ndiyo maadili ya kula chakula kwa mkono. Mtume ﷺ , siku zote, alikuwa akichota chakula kwa vidole vyake, tu, pasi na kuhusisha kiganja chake; tofauti na watu wengi, wenye kupiga matonge makubwa kabisa, kwa kiganja chote cha mkono, ambalo hawezi kulitia kinywaniu mpaka, kwanzaa, alikamue-kame na kulibinya-binya, ili liwe dogo la kuweza kuingizwa kinywani! Huo ni uroho na SI sunna ya Mtume ﷺ .
Kwa maana hiyo, mitindo yetu ya kuchota tonge kwa mkono wote, vidole vitano na kiganja cha mkono, na kisha KUIVIRINGA VIRINGA TONGE, ILI IWE NDOGO YA KUWEZA KUINGIA MDOMONI ni UROHO na KARAHA na wala SI MAADILI YA KULA. Hakuna haja, wala si busara, kuchota chakula kingi mkononi na kisha kukiminya minya ili kiweze kuingia kinywani! NI UROHO NA SI JAMBO LA KUPENDEZA. Mtume ﷺ hakupata kula kwa kuchanganya kiganja chake cha mkono kuchota chakula. Siku zote kiganja chake cha mkono kilisalia kikavu.
YALIYOMO NA YATOKANAYO
1. Ukamilifu wa unyenyekevu wa Mtume ﷺ katika kuwahudumia wake zake nyumbani.
2. Sunna kwa Baba mzazi kusaidia kazi za nyumbani, kadiri ya uwezo wake, na siyo kujigeuza mfalme Sulemani.
3. Hima ya Mtume ﷺ kudumisha Swala katika wakati wake, na kutokubali kushughulishwa na kitu chochote kengine, kufika hadi kuchelewesha Swala katika wakati wake.
4. Unyenyekevu wa Mtume ﷺ katika kuhudumia mambo ya Waislamu wenye kuhitajia zaidi, msaada wake; kama alivyosita kuhutubia ili kumfunza mpita njia aliyetaka aelimishwe kuhusu Dini yake, baadae kurudi kuendelea kutoa hotuba yake.
5. Umuhimu wa kumjibu, kwa haraka iwezekanvyo, mwenye kuuliza swali la Dini.
6. Wanazuoni wamesema kuwa ni Wajibu kumshughulikia mtu aliyekuja kuuliza kuhusu Imani na Dini yake, haraka iwezekanavyo na SI KUAHIRISHA hadi avunjike moyo. Kama alivyofanya Mtume ﷺ na mgeni huyu.
7. Kujuzu kukatisha hotuba, hata kama hotuba ya Ijumaa, ikitokea udhuru na dharura, na kisha kurudia kuondelea na hotuba.
8. Kukatisha hotuba kwa kutembea hatua chache, au hata kukaa kitako, kutokan na dharura, hakukatishi mfululilozo wa kisharia, hotuba yenyewe.
9. Sunna ya kula kwa vidole vitatu: Kidole gumba, kidole cha Shahada na kidole cha kaati.
10. Karaha ya kula kwa mkono mzima, kuanzia vidole vitano hadi kiganja cha mkono. Ni ishara ya uroho.
11. Sunna ya kula kwa tonge ndogo ndogo, na si kwa MATONGE MAKUBWA.
12. Suna ya kuramba vidole, BAADA ya kumaliza kula, na kabla ya kuosha mkono.
13. Chakula kikidondoka na kikawa kinaweza kuokotwa na kusafishwa, basi kiokotwe na kusafishwa na kisha kuliwa.
14. Kisicho safishika kisiokotwe na kuliwa; lakini kinaweza kuokotwa na kupewa wanyama wa kufugwa nyumbani, au hata wanayama wapita njia.
15. Sunna ya kuramba bakuli au sahani, baada ya kumaliza kula. Na kuramba huku ni kwa vidole na SI KWA ULIMI, kama anavyo ramba mbwa au paka.
16. Kujuzu kwa waliokula kwa pamoja kuramba sahani au bakuli, kwa vidole vyao na SI KWA NDIMI ZAO.
17. Kila chakula kina baraka iliyofichwa na Mwenyezi Mungu katika chakula hicho au chombo cha chakula hicho.
18. Hima ya Uwislamu na mafunzo yake katika kuhifadhi na kulinda neema za Mwenyezi Mungu.
19. Uharamu wa kumwaga chakula, kwa kisingizio kuwa ni MAKOMBO.
20. Uharamu wa kujaza chakula kwenye sahani, kupindukia uwezo wa walaji kumaliza chakula kile, kiasi kwamba kinachosalia kinatupwa!
21. Kuchunga n’gombe au mbuzi ni kazi ya Mitume, hivyo usimbeze mchunga wanyama.
22. Uhalali wa kupokea ujira kwa huduma halali uliyotoa.
23. Wajibu wa kuitikia mwaliko wa chakula, hata kama ni supu ya miguu ya mbuzi, isipokuwa kama una udhuru.
24. Sunna ya kumualika nduguyo kwenye chakula na Wajibu wa kukubali mwaliko huo; kwani jambo kama hilo ndilo linaloimarisha duguu na mapenzi kati ya watu wawili.
25. Kujuzu kufanya mashindano ya mbio na mfano wake: kama mbio za riyadha, pasi na kucheza kamari. Kwani kamari ni HARAMU.\
26. Kujuzu kumtunukia mshindi zawadi ya ushindi wake, ili kushajiisha mashindano kama hayo ya halali, BILA YA ZAWADI HIYO KUTOKANA NA KAMARI.
27. Kila mshindi ana siku atashindwa; na kila kipandacho juu kuna siku kitateremshwa chini. Hiyo ni KAWAIDA ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake.
28. Ukishindwa ukubali kushindwa, kwani hakuna kiumbe ambaye atashinda siku zote. Kukataa kushindwa, unaposhindwa, ni KIRUBI, hivyo ni HARAMU.
والله أعلم
وبالله التوفيق
السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم.
Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa Umma, ambacho ni tafsiri kamili ya رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام النووي kilicho tungwa na Imam An-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na Sayyid Abdulqadir Shareef Aal Shaykh Abi Bakr bin Salim آل الشيخ ابى بكر بن سالم.
NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza, na kuweka kwenye FB yako au kwenye WhatsApp na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com