KCWW. 51\6 MLANGO WA MATUMAINI

Hadithi za Marudio Jumamosi, tarehe 24 Mfungo Sita, 1446, sawa na 28 Septemba ‎‎2024.‎

KUHUSU KUWA NA MATUMAINI NA MWENYEZI MUNGU

SEHEMU YA SITA

‎51- Mlango wa Matumaini

Amesema Mwenyezi Munguسبحانه وتعالي ‏‎ :-‎

‎1.‎ Na rehema Yangu imeenea kila kitu (Al-A‘raaf, 7: 156)‎

‎434. Imepokewa kutoka kwa Jabir ‎رضي الله عنه ‏‎ akisema: Amesema Mtume ‎ﷺ ‏‎: “Mfano wa Swala tano [kuziswali kila siku] ni mfano wa kuwepo mto wenye maji ‎mengi, mbele ya mlango wa nyumba ya mmoja wenu, ambaye hukoga kwenye mto ‎huo mara tano kila siku.”Ameipokea Muslim. ‎

‎435. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbasرضي الله عنهما ‏‎ akisema: Nimemsikia ‎Mtume ‎ﷺ ‏‎ akisema: “Hatokufa Mwislamu akaswaliwa swala ya maiti na watu ‎arubaini, wasio mshirikisha Allah na kitu chochote kile, isipokuwa Mwenyezi ‎Mungu Atawakubalia dua zao njema wanazo muombea maiti huyo.”Ameipokea ‎Muslim. ‎

‎436.. Imepokewa kutoka kwa Ibn Mas‘udرضي الله عنه ‏‎ akisema: Tulikuwa ‎kama watu arubaini, hivi, pamoja na Mtume ‎ﷺ ‏‎ ndani ya kuba [hema la duara] ‎akasema: “Je, mtaridhika mkiwa robo ya watu wa Peponi?’ Tukasema: “Ndiyo!” ‎Akasema: “Je, mtaridhika mkiwa thuluthi moja ya watu wa Peponi?” Tukasema: ‎‎“Ndiyo!” Akasema: ‎

‎“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake! Mimi nataraji kuwa ‎mtakuwa nusu ya watu wa Peponi; kwa sababu haingii mtu Peponi isipokuwa ‎mwenye kuisalimisha nafsi yake kwa Mwenyezi Mungu. Na wingi wenu nyinyi, ‎kulingana na wingi wa wale wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, ni kama wingi ‎wa unyoya mweupe kwenye ngozi ya ng’ombe mweusi, au unyoya mweusi kwenye ‎ngozi ya ng’ombe mwekundu.” Muttafaq ‘alayhi. ‎

‎ ‎ ‎437. Imepokewa kutoka kwa Abu Musa al-Ash‘ariyyرضي الله عنه ‏‎ akisema: ‎Amesema Mtume ‎ﷺ ‏‎: “Itapofika Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Atamkabidhi ‎kila Mwislamu mmoja, Yahudi mmoja au Nasrani mmoja, na kumwambia: Huyu ni ‎fidia yako ya kuokoka na Moto.” ‎

Riwaya nyengine ya Abu Musa vile vile, inasema: “Amesema Mtume ‎ﷺ‎: ‎‎“Watakuja watu miongoni mwa Waislamu Siku ya Kiyama, wakiwa na madhambi ‎mengi, mfano wa milima, lakini Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zao hizo.” ‎Ameipokea Muslim. ‎

Amesema Imam Nawawi: Maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu: “Huyu ni ‎fidia yako ya kuokoka na Moto.” inaweza kueleweka zaidi kutokana na Hadithi ‎nyengine, iliyopokelewa kutoka kwa Abu Hurayra, isemayo: “Kila mtu ana makaazi ‎yake Peponi na makaazi mengine Motoni. Mwenye kuamini akiingia Peponi, basi ‎makaazi yake ya Motoni huchukuliwa na kafiri; kwa sababu anastahiki makaazi ‎hayo kwa ukafiri wake” Na maana ya “Fidia yako” ni kwamba: ulihatarika kuingia ‎Motoni na huyu ndiye fidia yako; kwa sababu Mwenyezi Mungu Ameshatuwekea, ‎tangu azali, idadi ya wataoujaza Moto. Hivyo, wakisha ingia makafiri Motoni, kwa ‎kufuru zao, wanakuwa kama wamewafidia Waislamu nafasi zao Motoni. Na ‎Mwenyezi Mungu anajua zaidi!‎

‎438. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Umarرضي الله عنهما ‏‎ akisema: Nimemsikia ‎Mtume ‎ﷺ ‏‎ akisema: “Mwenye kuamini atasogezwa karibu na Mola wake, Siku ya ‎Kiyama, mpaka afunikwe na rehema Zake, kisha Amhoji kwa madhambi yake; ‎Atamwambia: “Unakumbuka dhambi fulani na dhambi fulani?” Atajibu: “Ndiyo ‎Mola wangu! Nakumbuka.” Atamwambia: “Nilikusitiri nazo [nilikufichia] duniani, ‎na leo Mimi Nakusamehe na kukufutia.” Basi atakabidhiwa ukurasa wa amali zake ‎njema.” Hadithi zote hizi ni Muttafaq ‘alayhi

UFAFANUZI

Hadithi za sehemu hii zinaendelea kutufahamisha kuwa mwenye kumuamini, kwa ‎dhati, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hapaswi kukata tamaa na Rehema za ‎Mwenyezi Mungu, ilimradi tu anajitahidi kufanya amali njema, na kutaraji Rehema ‎za Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwa amali njema muhimu kabisa ni Swala ‎Tano za kila siku, ambazo anaye dumisha kuziswali, kila siku, hufutiwa dhambi ‎zake zote kama alivyosema Mwenyezi Mungu :‎
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ (هود,11 : 114 ‏‏) ‏‎ ‎
‎“Na dumisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu ‎na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao ‎kumbuka.” (Huud, 11:114). ‎

Hivyo, mfano wa kudumisha Swala tano kila siku, ni mfano wa mtu anayelazimika ‎kuogelea, mara tano, kwenye maji mengi yaliyopo mbele ya nyumba yake, kila ‎anapo toka au kurudi nyumbani, na hivyo kumfanya asafike na kila uchafu uliyopo ‎juu ya mwili wake. ‎

YALIYOMO NA YATOKANAYO

‎1.‎ Umuhimu wa kudumisha Swala tano kila siku.‎
‎2.‎ Kudumisha Swala tano kunapelekea kufutiwa madhambi yote madogo ‎madogo.‎
‎3.‎ Umuhimu wa Waumini walio hai kumuombea msamaha maiti Mwislamu.‎
‎4.‎ Shafaa, kwa aliyekufa, ni KUMUOMBEA na SI KUMUOMBA maiti! ‎Kumuomba maiti ni SHIRK!‎
‎5.‎ Swala ya maiti ni muhimu sana na ni Ibada ya kumuombea maiti.‎
‎6.‎ Umuhimu wa watu wengi sana kumswalia maiti; huenda pakapatikana, ‎miongoni mwao, watu 40 au zaidi, wasiomshirikisha Mwenyezi Mungu na ‎kitu chochote, na ambao wakimuombea msamaha watakubaliwa.‎
‎7.‎ Dua ya mja asiyemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote hairudi ‎mikono mitupu. Hivyo, ukikutana na mcha Mungu (yuhai kama wewe) ‎muombe akuombee dua!‎
‎8.‎ Maombezi ya mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote ‎hayakubaliwi.‎
‎9.‎ Wingi wa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa waja Wake, ‎ni sawa na WINGI wa manyoya ya ng’ombe mweusi, mwenye UNYOYA ‎MMOJA MWEUPE, mwilini mwake!‎
‎10.‎ Washirikina ni wengi sana kuliko Waumini halisi. Mwenyezi Mungu ‎Amesema: ‎‏ وما أكثر الناس ولو حرصت بمؤمنين ‏‎“Hata ufanye hima gani, bado ‎wengi wa wanadamu si watu wenye kuamini (ni washirikina).‎
‎11.‎ Dharura ya kuwa macho, kwa kila ulifanyalo, kuhakikisha ‎HUMSHIRIKISHI Mwenyezi Mungu na kitu chochote kile: khasa katika ‎KUOMBA!‎
‎12.‎ Waja wengi wataoingia Peponi watatoka kwenye Umma wa Muhammad ‎ﷺ ‏‎ ‎‎.‎
‎13.‎ Hatoingia Peponi ila mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu. ‎
‎14.‎ Bishara njema kwa Waumini wa Muhammad ‎ﷺ ‏
‎15.‎ Pepo na Moto zimeshaumbwa na Mwenyezi Mungu na kila moja itakuwa na ‎ujazo sawasawa wa idadi ya viumbe Vyake. (Yaani ukubwa wa kila moja ‎unaweza kuchukua viumbe vyote alivyo viumba Mwenyezi Mungu)‎
‎16.‎ Waliokufuru au kumshirikisha Mwenyezi Mungu, watatolewa kwenye ‎nafasi za ujazo wao Peponi, na walio muamini wanachukua nafasi zao ‎Peponi; vile nafasi za ujazo wao Motoni –kwa kumuamini Mwenyezi ‎Mungu- zitachukuliwa na wale walionyimwa nafasi zao Peponi, kwa ‎kumshirikisha Mwenyezi Mungu. [Ufafanuzi wa Imam Nawawi, ambao ni ‎sahihi, unatokana na Hadithi Swahihi aliyoinukuu katika Ufafafnuzi wake, ‎رحمه الله ‏‎)‎
‎17.‎ Dharura na umuhimu wa kuamini, na hatari na tahadhari ya kumshirikisha ‎Mwenyezi Mungu na kitu chochote.‎
‎18.‎ Fadhila za Mwenyezi Mungu kwa baadhi ya waja Wake, wenye kumuamini ‎kwa dhati, ambao atawasitiri duniani na Akhera.‎
‎19.‎ Kukiri kosa ni sawa na kuomba kufutiwa kosa ‎ألإعتراف يمحو ألإقتراف‎.‎
‎20.‎ Umuhimu wa kumsitiri Mwislamu kadiri iwezekanavyo.‎
‎21.‎ Mlango wa Toba upo wazi na ni mpana sana.‎

وبالله التوفيق ‏

الحقير إلى الله تعالى عبد القادر شريف آل الشيخ ابى بكر بن سالم

INAENDELEA….. ‎

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
Kutoka Kitabu cha: Kitalu cha Waja Wema: Maneno ya Muokozi wa Umma, ‎ambacho ni tafisri kamili ya ‎رياض الصالحين من كلام سيد المرسلين للإ مام النووي ‏kilicho ‎tungwa na Imam al-Nawawi na kufasiriwa kwa Kiswahili na Sayyid Abdulqadir ‎Shareef.‎
NI RUHUSA KUNUKUU NA kuweka kwenye FB yako au kwenye Whatsup na ‎kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.‎
kcwajawema@gmail.com

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *